• Active Topics 

Sitaisahau safari yangu ya Mauritius

Are you a good storyteller/writer, based on facts or created from imagination? Why not write here for us?
Post Reply
Joseph Bundala
Expert Member
Reactions: 23
Posts: 55
Joined: 7 years ago
Has thanked: 14 times
Been thanked: 28 times
Contact:

#1

Ilikuwa Jumatatu moja tulivu sana miaka kadhaa imepita sasa. Ni siku ambayo Simulink niliamka na kuanza kupanga safari yangu ni jinsi gani nitafika Mauritius baada ya maisha kuniwia vigumu sana. Motivation yangu ilichangiwa na usomaji wangu wa ramani ya Afrika katika somo la jiografia katika elimu yangu ya msingi. Pia na stori za kijiweni kuhusu ile nchi na ilivyo rahisi kupata kazi zisizo na elimu ya kutosha.

Nilianza uchunguzi kujua nitafikaje ingawa sikua na hela ya kupanda ndege bali nilikua na pasipoti tu. Baada ya kupiga chai chapati mbili na maharage kwa mama Kombo mtaani kwetu, nilipanda DCM kutoka napoishi mpaka feri kujaribu chunguza kama kunaweza kua na boti ya kunifikisha Mauritius au hata Anjuani Comoro. Nilikutana na jamaa mmoja pale feri alikua ni mfanyakazi kwenye kivuko cha kwenda Kigamboni. Alikua ni mzee wa makamo kapiga kizibao, aliitwa Musa. Nikamuuliza kama kwenye ile fukwe kuna boti ambazo zinafanya safari ya kwenda Mauritius. Alicheka sana, akanambia anachojua tu kuna boti za wangazija wanaotoka Anjuani ambazo zinabeba mizigo. Bahati nzuri kukawa na Mngazija naye anaulizia wapi anaweza enda nunua madawa ya binadamu (Pharmarcy) kwa jumla ili arudi nayo. Nikaona hii ni fursa, alijitambulisha kama Nawab, nikamweleza shida yangu akanambia hakuna tatizo huwa wanachukua hata abiria kwenye boti yao ila nauli ni elf 65. Akasema wanang’oa nanga baada ya siku tatu saa tisa usiku. Niliagana naye nikarudi zangu uswahilini kwetu.

Ile nauli kusema za ukweli ilinichanganya sana, nikasema kama Dar es salaam mpaka Anjuan ni elf 65, ntafika kweli Port Luis Mauritius?Hapo nilikua na akiba kama ya laki mbili tu kibindoni. Nikasema ngoja nipige mzigo nitafute balance ya kuongezea. Mungu mkubwa, nilienda dukani kwa Tarimo, huyu tulikua tunamuita ni saccos ya mtaa. Maana mtaa mzima ulikua kwenye rejesta yake ya madeni, nakumbuka hata siku moja alipigana na Mponda kisa hakurudisha hela aliyokopa mafuta ya taa. Nilimfata bila hiyana akanikopesha sh laki 3, nikaandika jina langu na sahihi mbele ya mjumbe wetu mzee Milanzi mwenyeji wa Kilwa. Tarimo akanambia ”Simulink, achaa ujingaa fungua duka wewe”

Asubuhi yake, nikaamka nasikiliza magazeti radio Tanzania. Nikawa nawaza altenative ya safari yangu ili kupunguza ile nauli ya elf 65. Kwa kuwa sikua na shughuli maalum ya kipato mchana ule nilienda kijiweni kupiga stori na washkaji. Kuna chinga mmoja yeye alikuwa na biashara ya mitumba kariakoo. Nikashangaa siku hiyo tulikua naye kijiweni, nikamuuliza kulikoni hujaenda? Akasema, mgambo walivamia bidhaa zao wakaharibu kila kitu ile jana yake, waliondoka hata na masufuria ya mama ntilie yaliyojaa wali. Akaanza sema anarudi kwao Rufiji bora akawe mvuvi wa majongoo baharini. Nikapuuzia shida zake baada ya kuniambia anarudi Rufiji, nikavuta picha naweza fika kisiwa cha Mafia halafu ntajua mbele kwa mbele kuelekea Anjuani au Mauritius. Nikamuuliza nawezaje fika Mafia. Akanipa ramani.

Ilikua ni kama saa nane mchana siku ya Jumatano, nilikuwa full maksinondo kama msolopagazi, full adrenalini kwa ajili ya safari yangu. Kama kawaida nikapiga wali maharage kwa mama Kombo, nikamwambia nasepa kutafuta maisha. Huyu mama ntilie aliniweka sana mjini kipindi nimechacha, maana hata ukoko sometimes nilikua nanunua kwake kwa sh 500 Tz. Nikapanda DCM mayai, ndani yake kibao cha C.R.E.A.M ”Cash Rules Everything Around Me” toka kwa Wu-Tang Clan kinapigwa na Abubakar Sadiki wa Radio One Stereohttps://www.youtube.com/watch?v=PBwAxmrE194 dollar dollar bill y'all. Nikashuka Mbagala rangi tatu kama saa tisa hivi, nikaulizia stand ya mabasi yanayoenda kusini. Nikaelekezwa, nikafika kwenye gari za Nyamisati nikalipia siti ilikuwa elf 4500. Sikutegemea kama ile gari ingekaa mda mrefu sana pale Rangi tatu, maana konda akasema gari itaondoka saa moja kasoro usiku. Nikamuuliza kama pale Nyamisati ntapata boti usiku huo, akasema kesho yake asubuhi ndio inang’oa nanga. Basi, safari toka Rangi tatu kupitia Mkuranga ikaanza, ilituchukua masaa matano kufika Nyamisati. Nilidhani ni lami tu, nikashangaa tunaitafuna changarawe tu kilomita kadhaa baada ya Mkuranga. Kwenye gari nikawa namuuliza konda kama kuna gesti za kulala hapo Nyamisati, tulipofika akanionyesha nyumba ya wageni. Nyamisati kimyaaa na giza balaa, wakati nafika hakukua na umeme mji mzima, nikaenda gesti nikalipia chumba elf 10. Nilikuwa na wasiwasi sana na usalama wangu maana niliamini labda wanapeana taarifa wageni waoingia wawapore. Ndani ya chumba, nikafunga mlango nikasogeza kitanda kwenye mlango mpaka asubuhi.

Nikafika pwani pale kwenye boti ya kwenda Mafia, nilichoka baada ya kuona ile boti. Boti imechoka balaa, nikawa naona wamewasha jenereta wanapump maji yatoke nje ya boti. Nikasema, hii safari hakuna kurudi nyuma. Nikalipia elf 12,500 Tz nauli, boti ikang’oa nanga kwenye mto Rufiji kuitafuta Bahari ya Hindi. Hapo pia nikapata kuona yale majongoo aliyokuwa anasema yule msela wangu chinga. Boti ilijaa naweza sema ni kupita uwezo wake, wanawake wote walikaa chini kwenye turubai, mimi kwa kuwa nilikua mgeni wa safari ya bahari, nilienda kaa mbele kabisa kwenye gati la mbao nikitaka kuona mandhari ya bahari. Lakini nilijutia uamuzi wangu ule, maana baada ya boti kuingia bahari kuu, mawimbi yalikua yanapiga pale kwenye gati nilipo mimi na kuingia ndani, abiria wote walijua mimi mgeni maana nilikua peke yangu pale kwenye gati. Nikapewa mfuko mweusi na jamaa wa ile boti, sikujua matumizi yake ila wakaniambia nikivurugwa na tumbo basi nitupie humo. Katikati ya bahari tukaona mbao zinaelea, nikasikia wenyeji wanasema kuna mashua iligonga mwamba ukanda ule na iliua watu wengi sana. Niliona hii safari bila hata navigation systems ni risk kubwa sana, maana niliona yule nahodha anaangali nje tu. Nikapata ujasiri maana safari ya masaa matatu baharini si mchezo kwangu, nikasogea kwa nahodha nikampa pakti ya sigara Embassy. Nikamuuliza anaendeshaje boti hana ile kampus, akasema mazoea tu, anafata nyota kule angani ambayo wameweka angle na mlingoti wa boti. Nilichoka baada ya kusikia vile, nikasema mbona siioni nyota? Akasema wasomi wanaiita Sayari ya Venus. Akanambia usiku nikipata muda niangalie angani kuna nyota inang’aa sana kuliko nyengine.

Tulifika Kilindoni Mafia yapata kama saa sita mchana hivi, safari ilikua ndefu kutokana na ukinzani wa upepo kuwa mkali sana. Mafia haikua na gati ya boti kutushusha, vilikuja vimtumbwi kutubeba mpaka pwani kwa gharama ya sh 500 Tz. Wakati niko pwani pale nakula vibua, nikamuona yule nahodha na tukaendelea kuongea ishu za safari yangu. Akanambia kuna usafiri wa kufika Anjuani ila Mauritius ni mbali sana kutokea Mafia. Akaniunganisha kwa mkaazi mmoja yeye ni mwenyeji wa Anjuani ana biashara zake pale Mafia. Nikaenda kulala gesti pale Kilindoni iliitwa New Lizu Guest House. Kesho yake asubuhi nikaenda kwa mzee Moulida Hassan ambaye ni mfanyabishara maarufu sana pale Mafia. Akanambia baada ya siku mbili kuna mashua itang’oa nanga pale Kilindoni kuelekea Anjuani. Nilifurahi sana kusikia hivyo na nauli haikua kali sana. Basi nikajiandaa na safari, nilifanya utalii kidogo wa ndani pale Mafia, nikafika Jibondo kuona wanao-dive kufata majongoo chini ya bahari. Jamaa mmoja anaitwa Sule nilishuhudia aki-dive kwa dakika ambazo mtu wa kawaida hawezi bila kuwa na Oxygen mask. Nikasema hii kazi naweza kufa huko chini. Maana katika somo la sayansi tuliambiwa unapozama kina cha chini zaidi ndipo mgandamizo wa hewa nao unaongezeka, ambapo unaweza chana mapafu na msukumo wa damu kuongezeka mara dufu.

Mungu mkubwa, baada ya siku mbili nikafika pwani kwenye mashua ya Waanjuani, nikashangaa mashua ipo mchangani pwani kabisa. Nikauliza tutaondokaje wakati mashua imenasa kwenye mchanga? Tatizo wale jamaa wanaongea kiswahili ambacho hakieleweki ila wako fluent kwenye French. Nikaanza nao mazungumzo kwa French yangu ya kuunga unga. ”Bon apres midi?, comment allez vouz monsieur”. Wakanambia nisijali mashua itaondoka baada ya maji kujaa wasomi wanaita high tides. Basi mida ya jioni wakasonga ugali pale pwani na dagaa kamba, sitasahau ule ugali maana niliula nikiwaza hii safari nayoianza ni ya hatari ambapo naweza nisirudi tena nchini kwangu. Tukapanda mashua usiku wa manane tukisubiri high tides walikadiria kama saa kumi na mbili asubuhi hivi. Mida ya saa moja hivi tanga likaachiwa juu ya mashua kuashiria safari yetu. Jamaa wakapiga dua pale tukaitikia Amiiiin. Sharti moja wapo nililokuta kwenye mashua ni kuvua viatu. Niliuliza safari inaweza tuchukua mda gani wakasema kama masaa tisa au kumi kulingana na upepo. Kwenye mashua walibeba nyama ya ng’ombe, mchele, mafuta ya kupikia, sabuni niliiona AYU na bidhaa yingi za majumbani. Nikapitiwa na usingizi.

Ghafla nikaamshwa, dah nikaona meli ya kivita imetusimamisha na imeelekeza mitutu kwenye mashua yetu. Ilikua inapepea bendera ya Marekani, nikaisoma ubavuni imeandikwa USS Nicholas-FFG-47. Wakaanza kuongea kiingereza kuwa tuweke mikono yetu juu, wakaingia ndani ya mashua yetu, wakaanza kukagua cargo za kwenye mashua. Bahati nzuri hakukua na madawa ya kulevya ama silaha zozote zile. Wakatuambia tunapita kwenye bahari kuu ambapo maharamia wa Kisomali wanateka sana meli ukanda huo mpaka wa ushelisheli. Wao walikua katika operesheni ya pamoja kulinda ule ukanda. Wakatuambia tuwe makini sana na sababu chombo chetu kinategemea upepo tu hivo tuko katika hatari kubwa sana ya kutekwa na wasomali. Wakatuacha wakaondoka, nilianza kutetemeka sana, maana maharamia hawana msalia Mtume. Jua lilikua kali sana mchana wa saa sita hivi, mawimbi yanapiga mashua inaegemea upande mmoja, nikaona vibarua wa ile mashua wanaamisha magunia ya mchanga upande ule mwengine kuibalance mashua ”Centre of Equilibrium”. Basi hali ikawa hivo kuhamisha tu magunia kutafuta centre of equilibrium. Ghafla upepo ukakata, wenyewe wanaita ”umsokheri” kwa kianjuani. Nahodha akasema ni hatari sana kwa mashua ku-sail bila upepo, ambapo inaweza sombwa uelekeo ambao hamuendi, akapiga hesabu zake akasema ikiendelea upepo kuwa vile basi tunaweza tokea pwani ya Mozambique.

Kweli bana, baada ya masa mengi sana mashua ikatia nanga pwani ya Msumbiji mkoa wa Cabo Delgado mji wa Pemba. Nilikua nimechoka sana na ile safari plus jua kali sana majini kuliko la nchi kavu. Evaporation unaisikilizia sana tu. Na niliweza prove ile theory dunia ni duara kwa kuangalia CIRCUMNAVIGATION. Maana mashua inapoenda unaona kama unaikata curve flani hivi ya sphere kwenye bahari. Pale Cabo Delgado nikaulizia kama kuna Watanzania, nikakuta wengi tu pale wanafanya biashara. Nikaseto kwa miaka miwili nikifanya ishu za madini ya rubi. Nikatafuta chotara wa kireno nikarudi naye Tanzania kupitia boda ya Mtwara, nikachukua basi la Akida mpaka Dar es salaam nikaendelea na maisha ila mreno alirudi kwao baada ya sintofahamu za hapa na pale. Sitaisahau safari yangu ya Mauritius ambako sikufika.

Author: Simulink
0
User avatar
Eli
Senior Expert Member
Reactions: 183
Posts: 5211
Joined: 9 years ago
Location: Tanzania
Has thanked: 75 times
Been thanked: 88 times
Contact:

#2

Umenikumbusha mbali, hasa kuhusu kipindi kimoja kilichokuwa kinaendeshwa Radio Free Africa, "Sintosahau". Kilikuwa kinaendeshwa siku ya Jumapili, nadhani kuanzia saa tatu asubuhi na kurudiwa siku nyingine. Kilikuwa ni kipindi cha simulizi za kusisimua sana kuhusu safari mbalimbali za vijana wakijaribu kuchanja mbuga kuelekea South Africa na sehemu zingine ili kutafuta Maisha. Wengi safari zao zilionekana kuanzia Dar Es Salaam, kama ni kwa kuzamia meli, kutokea bandari iliyopo Kurasini au kwa boat kuelekea pwani ya Mtwara na kuingia Msumbiji.

Waliokuwa wakitumia barabara walipitia Tunduma, na kuingia Zambia - Zimbabwe, na pengine Botswana hadi South Africa. Safari zao zilionyesha kuambatana na hatari nyingi sana. Jamaa mmoja alieleza jinsi walivyofanikiwa kuingia South Africa kupitia pwani ya Msumbiji wakiwa kwenye boat, hawakuweza kupitia nchi kavu kwa sababu hawakuwa na passports. Alieleza jinsi walivyokumbana na hatari mbalimbali ikiwemo kunusurika kuzamishwa baharini na maharamia. Huku wakiwa wamevuka viunzi vingi, waliingilia South Africa kupitia mbuga ya wanyama ya Kruger, lakini walimpoteza mwenzao mmoja kwa kudakwa na mamba wakati wakivuka mto Limpompo.

Safari zao zilikuwa kama vile za kufikirika, kwa sababu wengi walikuwa wakiondoka nchini huku hawana kitu mfukoni.

Kuna mwingine alisimulia jinsi alivyozamia Congo na kujikuta yupo msituni. Baada ya kusota sana alibahatika kukutana na kikundi cha wawindaji porini wakiwa wamebeba nyama. Aliweza kuelewana nao na baadaye walipika na kula. Alikula sana nyama kwa sababu ya njaa, ila baadaye akagundua kumbe nyama aliyokula ilikuwa ni ya nyani!

Maisha ni safari yenye milima na mabonde!
0
TSSFL -- A Creative Journey Towards Infinite Possibilities!
Post Reply

Return to “Story Writing, Fiction and Nonfiction”

  • Information
  • Who is online

    Users browsing this forum: No registered users and 0 guests